ZIKIWA zimesalia siku 11 kabla ya lile tamasha kubwa la ujasiriamali linalosubiriwa kwa hamu la Street University halijafanyika, kundi la muziki wa Injili la Dot Com Generation limeahidi kuifanya Arusha ichimbike kiburudani.
Tamasha hilo litakalofanyika Novemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja vya Sheikh Amri Abeid litawapa mbinu za kupata utajiri wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani. Mbinu hizo zitamwagwa na wajasiriamali wa kimataifa, Eric Shigongo na James Mwang’amba.
“Tutahakikisha wajasiriamali watakaohudhuria wanaburudika vya kutosha kwa nyimbo zetu kali kabla ya kuanza kupokea somo kutoka kwa wataalamu wetu, Shigongo na Mwan’gamba,” alisema kiongozi wa kundi hilo, Martin Bashando.
Naye mratibu wa tamasha hilo, James Mwang’amba alisema hiyo ni fursa kwa wafanyabiashara wa Arusha kujifunza namna ya kukuza mitaji na kupata utajiri ndani ya muda mfupi, kujikomboa na umaskini kupitia biashara, namna ya kupata mawazo ya kibiashara na jinsi ya kuomba na kupata mikopo mikubwa benki.
Tamasha hilo litasindikizwa na burudani kabambe kutoka kwa wasanii wa muziki wa Injili na kizazi kipya Bongo, Christina Shusho, Bonny Mwaitege, Abass Hamis Kinzasa ‘20%’, Glorious Singers na wengine wengi kwa udhamini mkubwa wa Kampuni ya Global Publishers Ltd, Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Umma (PSPF), Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Wafanyabiashara na Wakulima (TCCIA) na Hoteli ya Kibo Palace ya jijini Arusha.
Wadhamini wengine ni Tripple A Radio (88.5 FM), Sunrise Radio (94.8 FM), Mambo Jambo Radio (93.0 FM) na Radio 5 (105.7FM), zote za jijini Arusha.